MONICA

July 22, 2018

Monica alikuwa ni msichana mrembo sana, kila aliyemtizama alivutiwa na urembo alionao, na hata yeye alijitambua kuwa ni mrembo. Katika maisha yake Monica alikuwa anapenda sana vitu vizuri na vinavyokwenda na wakati kama nguo, viatu, simu na vitu vingine kadha kwa kadha. Lakini wazazi wake walikuwa hawana uwezo wa kumnunulia vitu vyote hivyo.

Baada ya kumaliza kidato cha nne, kwa bahati mbaya hakufanikiwa kuendelea na kidato cha Tano na hivyo wazazi wake waliamua kumtafutia chuo.Akiwa anasoma chuo alikutana na marafiki wa aina mbalimbali na marafiki zake wakubwa walikuwa ni wale ambao wametokea katika familia ambazo wanajiweza yaani matajiri. Kutokana na wazazi wao kuwa na pesa walikuwa wakimiliki simu nzuri, na kompyuta (laptop) lakini kwa upande wa Monica alikuwa hana hata simu ya mkononi, alitamani sana kuwa na maisha mazuri kama ya wenzake.

Siku moja akiwa anatoka chuo kuelekea nyumbani alikutana kaka mmoja aliyekuwa anaendesha gari aina ya Altezza “Mambo mrembo, unaelekea wapi mamii” Yule kaka alimwita Monica huku akipunguza mwendo wa gari lake. Monica alimtizama yule kaka na kusema “Hapana asante, nitapanda tu daladala” Yule kaka akaendelea kusema “Samahani lakini mrembo,nakuomba mara moja kuna jambo nilikuwa nataka nikuulize” Basi Monica akasogea karibu “Uliza tu hakuna tatizo” Kumbe yule kaka alimwita kwa ukaribu ili ambembeleze apande kwenye gari yake. Haikupita muda Monica alikubali kupanda kwenye lile gari na waliendelea kuzungumza na kufahamiana.

Yule Kaka alikuwa ni mfanyabiashara, anaitwa Abdon.Kutokana na Monica alikuwa hana simu ya mkononi Abdon alimuahidi kumnunulia simu, na kesho yake angempelekea pale chuoni. Baada ya kumfikisha Monica maeneo ya nyumbani, alimpatia kiasi cha shilingi elfu hamsini “Kiasi hiki kidogo cha pesa kitakusaidia, kwa nauli siku ya kesho, nimefurahi sana kukufamu Monica, wewe ni mrembo ukinipa nafasi katika moyo wako, nakuahidi utafurahi sana” Monica huku akiuma vidole vyake kwa aibu akapokea ile pesa na kusema “Asante sana Abdon, ila naomba ukanishushe kwa pale mbele hapa Mama akiniona itakuwa balaa” Basi akasogea mbele kidogo na kumshusha.

Monica alikuwa anatabasamu huku akizungumza na nafsi yake “Jamani, leo ni siku yangu ya bahati, huyu kaka anaonekana ni mtu mwenye pesa sana, yaani amenipa shilingi elfu hamsini ijapokuwa sijamjibu chochote kuhusu ombi lake, mmmh yaani huko chuoni watanikoma, kwanza hii pesa niifiche vizuri, nikienda Mwenge nanunua viwalo kwa kwenda mbele” Siku hiyo Monica alikuwa na furaha sana. Kesho yake kama kawaida alikwenda chuoni, alipotoka tu alimkuta Abdon anamsubiri.

Moja kwa moja walisalimiana na alimpakia katika gari lake wakiwa ndani ya gari Abdon alimpa Monica simu nzuri ya mkononi aina ya samsung galaxy. Monica kwa furaha alimkumbatia Abdon huku akimbusu na kusema “Asante sana, jamani nimefurahi sana, kweli nimeamini unanipenda Abdon” Huku akicheka Abdon akasema “Nimekupenda sana Monica, ukiwa na mimi kila kitu unachokitaka utakipata nipo kwaajili yako”.Na huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa mahusiano ya kimapenzi kati ya Monica na Abdon.

Maisha ya Monica yalibadilika, kwani alianza kuvaa nguo za gharama na alikuwa hapandi daladala tena sasa alikuwa akijakuchukuliwa na kupelekwa chuo kila siku. Na hata wazazi wake walipokuwa wakimuuliza na kumkanya alikuwa awasikilizi aliwadharau na kuona Abdon pekee ndiyo wa muhimu katika maisha yake. Aliishi maisha ya starehe sana na kuwadharau watu wengine bila ya kujali chochote. Hata marafiki zake walikuwa wakimshangaa “Mmmh ama kweli watu wanabadilika, sikuhizi Monica anaringa sana tokea ampate huyo bwana mfanyabiashara” Walikuwa wakizungumza marafiki zake.

Baada ya miezi sita Monica alipata ujauzito na kuamua kumwambia Abdon ambaye alimwambia asijali atamlea vizuri. Basi akawa na kiburi kuwa ataolewa na Abdon. Baada ya siku mbili tatu Monica akiwa hana hili wala lile, mara alipita muuzaji wa magazeti na moja kati ya yale magazeti ukurasa wa mbele kulikuwa na picha ya Abdon na habari ikisema “Mfanyabiashara jambazi asotwa rumande” Monica hakuamini alichokiona akasogea karibu na kununua lile gazeti kisha kusoma kwa umakini. Ni kweli habari ile ilimuhusisha Abdon kutokana na kosa la ujambazi.

Akiwa anaendelea kusoma ile habari akagundua kuwa Abdon alikuwa na mke na watoto watatu. “Mungu wangu, inamaana Abdon ni jambazi, na tena kumbe alikuwa na mke? Mama yangu nimekwisha.Nitafanya nini mimi na nina mimba ya miezi minne sasa na nyumbani lazima nitafukuzwa najuta mimi TAMAA IMENIPONZA. Alikuwa anaongea mwenyewe kama mtu aliyechanganyikiwa.

Baada ya mwezi mmoja kupita hali ilizidi kuwa mbaya kwani mawasiliano na Abdon hayakuwepo tena. Na sasa aliwaomba msamaha wazazi wake na bila hiana wazazi walimsamehe.Hivyo walimlea hadi alipojifungua salama mtoto wa kiume. Na maisha ya Abdon haikueleweka yaliishia wapi kwani watu wengine walikuwa wanasema kuwa baada ya kuachiwa huru alihamia nchi nyingine pamoja na familia yake.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

4 × three =