Mimi na Wewe tutaondokaje hapa Duniani.?

July 22, 2018

Ukweli ni kwamba kuna siku nitalala milele, sitaamka tena. Maisha yangu hayatakuwa ya hapa duniani, nitarejea kwa yeye muumba wa mbingu na ardhi.

Matendo pekee ndiyo yatakayonichagulia makazi ya kuishi, kati ya pepo na moto, kati ya mbingu na kuzimu, kati ya kwa waastarabu na watukutu. Yapi yatakuwa makazi ya milele kwangu.?

Nitawaacha ndugu, jamaa na marafiki wakibubujikwa na machozi, nitamuacha Mchumba, Mke/Wake, Mama, Baba au rafiki wakishindwa kujizua juu ya uchungu wa kifo changu. Wote watakuwa wa kuangua vilio tu.

Wapo watakaolia na kusaga meno, wapo watakaocheka na kufurahia kifo changu, inawezekana kuna watakaofikia hatua ya kucheza muziki na kula vizuri kwa kifo changu. Hii yote inaweza kutokea katika maisha ya mwanadamu yeyote.

Nitaacha kuzungumzia SOKA, Sitoweza kutaniana na watu, Sitoweza kaundika chochote TL na kwingine, Sitoweza kushiriki katika majukwaa #ElimikaWikiendi , #TwitterGulio , #VijanaNaAmani n.k lakini hamtaacha kusoma niliyoyaandika kabla ya kifo kunikuta. Siijui siku wala saa, lakini nitarejea kwake.

Ndugu yangu  amesema yeye ataiacha ofisi yake ikiendelea na kazi zake, anaweza kuja mwingine kuchukua nafasi yake. Atawaacha marafiki zake wacheza soka wakiendelea kuonyesha vipaji vyao.

Nitaacha kabisa kupiga Picha sehemu mbali mbali, kwenye events na sehemu zingine, Nitaacha vifaa vyangu, Sijui nani atavitumia, Nitaacha washikaji zangu ambao tulikuwa tunapendana sana na kusaidiana katika kila hali. Nitaacha kabisa kuendesha baisikeli yangu muda wa mazoezi.

Nitaachana na kukutana na msongamano wa magari na kubanana kwenye daladala na watu wa aina tofauti tofauti, waliokuwa makini kuliko mimi au waliopotea kuliko mimi, Sitoweza kunywa Juice ya Miwa tena. Sitoweza kupata Biriani kutoka @MgahawaCafe , Ugali na Pweza kutoka @pwezacafe

Nitaacha watu wengi ambao kuna kidogo walikuwa wanajifunza kutoka kwangu, Hawatapata muda wa kujifunza kipya kama nikishaondoka labda wataendelea kunufaika na kile nilichokiacha kipindi kile wakati ningali hai. Sitoweza tena kujifunza mambo mengi kutoka kwa watu mbali mbali.

Huwenda nikamuacha mama yangu pekee akiwa na machozi katika mboni zake za macho, kama atakuwa hai siku hiyo. Hakuna anayejua kati yangu na wewe unayenisoma nani atawahi kutangulia kwa manani.

Kuna mambo mawili tu makuu duniani, kuishi mara moja na kufa mara moja, hakuna lingine zaidi ya hivyo, hayo mengine ni nyongeza. Kama tulizaliwa ili tufe, tunashindwa vipi kufa ili tuishi.? Lazima tutarudi kwake.

Kiburi, kujiona na dharau havitatufikisha tunapofikiria kufika. Kama maandiko Matukufu yamekataza, sisi nani katika ulimwengu huu tuvitukuze? Kuna siku hatutokuwepo duniani hakika.

Utu, moyo wa kusamehe, kujishusha na kukubali makosa ni miongoni mwa mambo yatakayotuweka huru duniani, lakini ibada, kufanya toba na kuacha yaliyokatazwa na Mungu, ni miongoni mwa yatakayo tufanya tukapata makazi bora baada ya kufa. Mwisho wa siku atabaki Mungu pekee.

Ni kujitafakari. MIMI/WEWE Tunaondokaje.?


Comments

  1. John - July 22, 2018 at 20:01 - Reply

    Ujumbe mzuri, hakika binadamu tu mavumbi na mavumbini tutarejea. Yatupasa tuishi kwa upendo tuwapo hapa duniani.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

eighteen − 4 =