Binti wa darasa la Sita aliyemgusa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

February 25, 2018

Ndugu zangu wapendwa,

Huyu ni Noela binti mwanafunzi wa darasa la sita huko Kisorya wilaya ya Bunda mkoa wa Mara.

Wakati Mheshimiwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiwa Kisorya akizungumza na wananchi, nikanong’onwa nigeuze macho kwa binti mmoja kadogo kako mbele ya umma mkubwa uliokuwa unamsikiliza Mhesh WM. Kitu kilicho tuvutia kwa mara moja ni jinsi binti huyo alivyokuwa anasikiliza kwa umakini hotuba ya Mheshimiwa WM na kuandika yaliokuwa yanasemwa kwenye daftari lake la shule.

Image may contain: 1 person, sitting

Nikishindwa kujizuia, nikamsogelea kiaina kwa kuzingatia kwamba nisigeuze macho ya watu nje ya hotuba wa WM. Kimya nilipomfikia nilichungulia kwenye daftari lake na kwa mshangao mkubwa nikakuta kwa hati safi kabisa amenukuu yote yaliokuwa yanasemwa na Mhesh WM. Nilishindwa kujizuia na nikavunja itifaki zote na kumpeleka binti huyu kwa Mhesh WM akamsalimie lakini pia na yeye binti huyo apate kumbukumbu ya siku yake hiyo.

Nilipomsimulia Mhesh WM kuhusu binti huyu Noela tukavunja itifaki zote naye akaanza kumhoji kabinti na kumuomba amuazime daftari lake hilo. Kama mimi Mhesh WM naye akabaki amepigwa butwa kutokana na umahiri na umakini wa namna binti wa darasa la sita alivyokuwa ameandika hotuba yake. Ninaamini kwamba hata baadhi ya wasaidizi na waandishi wa habari wangeweza kumuomba Noela daftari lake na wakawa wamemaliza kazi kwa siku hiyo.

Image may contain: 1 person

Tangu nimeteuliwa na Mhesh Rais kuwa Mkuu wa Mkoa wa MARA nimepigia kelele sana suala la ukatili wa jinsia na haswa ubaguzi na ukatili kwa watoto wa kike. Nimesema mara kadhaa kwamba hakuna jamii ya watu inayoweza kuondokana na umasikini na kuyafikia maendeleo ya kweli na mabadiliko chanya ya kiuchumi, kijamii na kisiasa kama mabadiliko haya hayamshirikishi kwa upana Mwanamama, Mwanamke, Mwanadada!!!

Kuamini kwamba maendeleo yanaweza.kufikiwa kwa kuwakandamiza akina mama na kuwabagua wasichana kwenye elimu na mfumo wa jumla wa fursa za maisha ni umaskini wa akili, ambao ni umaskini mkubwa na.mbaya zaidi kuliko hata umaskini wa kipato! Ndio maana sisi wana Mara tunahimizana kuondoa kabisa tabia hizi za ukatili na ubaguzi wa watoto wa kike kwa kauli mbiu yetu ya ‘ Hatukubali katika Mara yetu’!!

Image may contain: 2 people, people standing

Nakushukuru Kabinti Noela.kwa kutukumbusha sisi sote, na kwa kuwa mfano hai wa uwezo wa watoto wa kike na umuhimu wa kuwafungulia fursa sawa. Wewe ni chachu kwa sisi wote kujituma zaidi ili kufanya makubwa zaidi

Asante sana Noela, na Mwenyezi Mungu akunyanyue juu zaidi uwe kiongozi wa sisi wote, na uendelee kuwa mfano, Mungu akubariki

Wako

Adam Malima


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!