“Hakika nilikosea sana kukuamini, Umeharibu maisha yangu”.

February 5, 2018

Inasikitisha sana Hii ni barua ya Fausta kwa aliyekua mumewe……

” My X Husband,

Nilikuwa binti mdogo ambae nilikuwa nikisoma chuo kikuu nikiwa na mipango mingi ya kimafanikio na malengo mengi baadae. Ndipo ulipokuja katika maisha yangu.

Nilikutana na wewe na nikakupenda, ulionekana ni mtu ambae mwenye mapenzi ya kweli, mtu unae jali na ambae hutaniacha nidondoshe chozi hata siku moja. Pamoja na hayo yote ulionekana pia u mcheshi ambae usingeacha tabasamu lipotee usoni mwangu. Hakika ulikua Mwanaume kila mwanamke angependa kuolewa nae!

Tulifungua ukurusa wetu wa uchumba, nilikupenda sana na na nadhani unalijua hilo mpaka kesho, ulinisisitizia sana suala la kufunga ndoa mapema kwani ulikua ukiniambia kuwa una wivu, kwamba wanaume wengine wanaweza wakakupiga counter attack na kunioa kisha nikuache wewe kwenye mataa.

Mimi nilisita sana hilo suala, nilikusisitizia kuwa uniache mpaka nimalize masomo yangu ya chuo kikuu kwani ilikuwa imebaki miaka miwili tu, vilevile nilikueleza kuwa wazazi wangu wasingekubaliana kabisa na hilo wazo lako! Lakini wewe hukunisikia! Ulibaki na msimamo wako wa kutaka kufunga ndoa na mimi, kwamba ningeendelea na chuo baada ya ndoa.

Mwanamke gani ambae angekuwa tayari kukupoteza wewe? Bila kufikiri nilikubali unioe na niliwaeleza wazazi wangu hilo suala. Nakumbuka wazazi wangu walikuja juu sana, hawakutaka kunielewa kabisa!! Waliniuliza mara kumi kumi huyo mtu umemchunguza kweli? Mimi niliwahakikishia asilimia mia moja kuwa wewe u mwanaume unaepaswa kunioa!

Nilikuwekea dhamana ya uaminifu kwa wazazi wangu, na kwa vile mimi ndiye nilikuwa mtoto wao wa kwanza na wa kike pekee walinisikiliza na kutaka niwe makini nikuchunguze vizuri. Hilo halikunipa wasiwasi! Nilishakupenda na niliona wewe ndio mtu sahihi wa kuanzisha familia pamoja. Nilikupenda na sikuona tatizo lolote.

Vikao vilifanyika pande zote bila tatizo lolote, ulinioa mume wangu tena kwa sherehe ya harusi kubwa pale mjini, ilihudhuriwa na watu wengi sana ambapo mimi sikufikiri kama ingalikuwa vile. Tuliingia rasmi katika maisha ya ndoa!

Maisha ya ndoa yalinoga, mimi malkia ulikuwa ukiniambia kuwa unanijali sana na kweli ulinijali, kwamba maisha yako bila mimi si kitu…kweli ulinipenda, unaweza usikumbuke maneno matamu uliyokuwa ukiniambia lakin yote mimi nayakumbuka na bado yapo kifuani pangu! Niliacha marafiki zangu, familia yangu, mkoa wangu, nikabadilisha hadi jina langu na kutumia lako hii yote kwa ajili yako tu!

Taratibu ukaanza kubadilika, ukaanza kuniambia kwamba siwezi kuendelea kusoma, nililalamika sana na bila kugundua kuwa ulikuwa ukivunja ahadi yako. Ulinilazimisha niache chuo, pasina kujua kufanya vile ni kukosa kabisa mkopo wa elimu ya juu huko mbeleni, sijui ulikuwa na roho gani mbaya ilikuingia! Ukaanza kuwa na hasira na mimi! Hukuisha kunitukana na kunikebehi kila uliporudi toka kazini! Ulininyanyasa pasina kuwa na huruma kuwa nilikua nimebeba kiumbe chako tumboni mwangu.

Nilikuwa mpole, muda mwingine kosa ulikua ukifanya wewe ili kuepuka shari nikawa nikiomba samahani mimi. Mume wangu ulibadilka! Ukawa unarudi nyumbani usiku sana huku umelewa! Ulitukana matusi yote nayoyajua hapa duniani. Ukaenda mbali zaidi na kuanza kutembea na wanawake hovyo hovyo! Najiuliza mpaka leo! Ni kwamba sikukuchunguza vizuri au ni wewe tu ulichukulia ndoa kama mchezo wa kuigiza.

Tena nakumbuka mimba ilipofikisha miezi nane uliniambia hunipendi kabisa, kwamba hukutaka kunioa mimi, kwamba nilikuwa manamke kwanza mbaya, mpumbavu na mzigo kwako hayo yalikuwa maneno yako. Na kwamba unampenda mwanamke mwingine. Nilijihisi kusalitiwa sana sio siri uliniumiza sana ila sikufikiria kukuacha! Nilijipa matumaini tu kuwa utakuja kubadilika na kurudi kama zamani.

Lakini haikuwa hivyo mpaka pale ilipofika wakati niliposhikwa na uchungu nikiwa peke yangu nyumbani wewe ukiwa baa unakunywa pombe! Nilikupigia simu uje unichukue na gari yako kwamba ninakaribia kujifungua unipeleke hospitali lakini ulinijibu kwamba niache usumbufu upo unakunywa na warembo! Ulikuwa na roho gani mume wangu???

Majirani zangu ndio walikuja kunichukua baada ya kusikia kelele za kuomba msaada, walinipeleka hospitali na nikajifungua kwa operation mtoto wa kike! Nilishukuru Mungu kwa zawadi ya mtoto, ila nilisikitika kwa zawadi nyingine ambayo ulinipa! Zawadi ya ugonjwa wa UKIMWI! Inaniuma mume wangu! Umeharibu malengo yangu!

Uliniachisha chuo, ambako nilikua ninaenda vizuri na masomo yangu ya udaktari, ulinitenganisha na rafiki zangu, ndugu zangu na familia yangu! Alimradi niwe na wewe tu.

Haikutosha umenizawadia na gonjwa la UKIMWI! nasema asante sana mume wangu, nina maumivu mno! Kwanini usingeniacha niendelee na masomo yangu kisha ndio unioe!? Kwanini ulikuja katika maisha yangu? Wewe tu ndiye uliyeharibu mipango yote ya maisha yangu. Asante sana Mume wangu.

Bado nipo katika kipindi kizito cha kutibu hii shock uliyonipa na sijui kama nitafanikiwa kurudi katika maisha yangu ya kawaida. Bora ungenichoma kisu nife kabisa kuliko haya maumivu uliyoniachia!

Lakini napenda tu nikuulize kwanini umeharibu maisha yangu? Siku zote za furaha tulizokua pamoja hazikumaanisha chochote kwako? Je taasisi ya ndoa ni kama utani kwako?

Najua maisha yako hayatabadilikia, bado u kijana mtamashati, handsome na mwenye pesa, lakini mimi na familia yangu ndio tunahangaika sana mimi ndio nlikua tegemeo lao kubwa sana. Sitakuja kuelewa kwanin ulinioa. Sina hasira na wewe ila nimeumia sana kwa kuharibu maisha yangu na ya familia yangu kiujumla. Nimeumia pasina kufananisha na maumivu yoyote yale.

Usijali kuhusu binti yangu mimi nitamtunza! She is my daughter!

Wasaalamu,

X-wife wako! FAUSTA”
****************
.

UJUMBE WA FAUSTA KWA MABINTI NA WANAWAKE KWA UJUMLA

1. Ombeni sana Mungu awaepushie wanaume washenzi kama huyu
2. Kuweni makini msiwe wepesi kutekeleza maagizo ya wachumba au waume zenu pasipo kutafakari madhara yake mbeleni 
3. Mume anayekusaliti na kukutesa bora kuwahi kuachana nae kabla hajakuletea magonjwa 
4. Sikilizeni ushauri wa wazazi na wazee kwan mara nyingi wao huwa na uzoefu zaidi kuhusu ndoa na maisha kwa ujumla

Ni matumaini yangu kwamba umejifunza kitu kupitia mkasa huu,

Nakutakia siku Njema, Mungu Akubariki na kukulinda


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!