Ahsante Ronaldinho Gaucho kwa kuniachia cha kuwasimulia wajukuu zangu.

January 17, 2018

TAZAMA VIDEO HAPA:

SOMA:

 

Anaandika: Jalilu Zaid

Na kusimulia:  Jalilu Zaid

 

Zama mbali mbali za Wacheza soka zimepita, katika historia ya mpira wa miguu na zingine tukiendelea kushuhudia vipaji lukuki vikiibuka kila iitwapo leo. Walikuwepo akina Edson Arantes almaarufu kama Pele na Diego Armando Maradona Franco wengi hupenda kumuita Diego Maradona ambaye inakumbukwa aliwahi kufunga goli yeye akaliita goli la mkono wa Mungu. Wote hawa na wengine kibao walitikisha ulimwengu kwa nafasi zao katika soka.

Ilikuwa siku ya ijumaa harufu ya wikiendi imeanza kutanda katika kila kona ya nchi ya  Brazil tarehe 21 mwezi wa tatu ya mwaka 1980 alizaliwa kijana mmoja ndani ya jiji la Porto Alegre almaarufu kama (Joyful Harbor) katika nchi ya Brazil. Kijana huyo nani tena.? Ni Ronaldo de Assis Moreira maarufu kama Ronaldinho Gaucho, wengi hupenda kumuita Gaucho. Maana ya Gaucho unajua ni nini.? Waingereza wanasema GAUCHO is a person who takes care of male and female cows.  Lol! Balaa hili sasa msakata kabumbu na kuchunga hao ng’ombe kuna uhusiano gani.? Labda wao wana maana yao nyingine tu.

Kama ilivyo kawaida kwa kila mtu mtoto akizaliwa katika familia fulani inakuwa ni furaha kubwa sana kwa sababu ya mapokezi ya kiumbe kipya ambacho hawajui kesho au keshokutwa huyo mtoto aliezaliwa atakuja kuwa nani katika ulimwengu hivyo nina uhakika hata familia ya mzee Moreira haikujua kabisa kama Ronaldinho angekuwa hivi tunavyomzungumzia sasa hivi. Waliobahatika kufika Brazil huwa wananipa stori wakisema ukikatiza katika mitaa ya Brazil huwezi kukosa watoto wadogo wakicheza soka katika mitaa hiyo, wao huita samba sisi kikwetu kwetu twaita “Gozi”. Maisha ya aina hii Ronaldinho nae aliyapitia ambako akiwa na miaka 7 tayari alianza kuwa gumzo katika mtaa wao kutokana na uwezo wake.

Kama ilivyo kwa wanasoka wengine wa Kibrazil, Ronaldinho Gaucho naye alianza soka lake kwa kucheza samba mtaani kwao Brazil baadaye akaonekana na kupelekwa katika klabu ya Gremio alikoanza kuvaa viatu. Alijulikana kutokana na ujuzi wake pamoja na ubunifu; kutokana na wepesi wake awapo na mpira, kasi na uwezo wake, pamoja na matumizi yake ya mbinu tofauti.  Wengi wetu tumemuona Gaucho tangu kila mechi aliyokuwa akicheza basi yeye ni wa kuwa natabasamu tu usoni mwake. Meno yake yaliyopangiliwa vizuri kinywani mwake hakuacha kuyaacha nje huku akionesha tabasamu hata ikitokea mchezaji amemchezea rafu basi yeye hakuwa ni mtu wa kuonesha hasira usoni yeye alikuwa akiwaadhibu kwa kanzu na vyenga maridadi ambavyo ilikuwa ni adhabu tosha kwa wacheza rafu kwake. Siku ni moja ambapo mimi pamoja na ulimwengu mzima tulimshudia Gaucho akitoa machozi uwanjani.

Ronaldinho alianza kulia baada ya kufunga goli. Muda huohuo akapiga magoti na kuanza kulia huku wachezaji wenzake wakiwa wamemzunguka.

Lilikuwa ni tukuio la kushangaza, hasa kutoka kwa mchezaji maarufu wa aina yake ambaye hutabasamu muda wote akiwa uwanjani.

Kilio hicho kilitokana na majonzi aliyokuwa nayo Ronadinho kutokana na kufiwa na baba yake wa kambo aliyefariki siku chache kabla ya mchezo kutoka na shambulio la moyo (heart attack). Hii ilikuwa kipindi anacheza Atletico Mileiro.

Mwaka 1998 kwa mara ya kwanza Ronaldinho Gaucho alianza kuichezea klabu ya soka ya Grêmio ambako alidumu pale mpaka mwaka 2001. Alifanikiwa kuichezea michezo 52 na kufunga magoli 21 katika michezo yake hiyo.

Ilipotimu Mwaka 2001 matajiri wa Jiji la Paris nchini Ufaransa Paris Saint German waliamua kumsajili Ronaldinho Gaucho na wakamchukua tayari kuwatumikia ambako alidumu pale kuanzia mwaka 2001 mpaka 2003  na baada ya Hapo ilikuwa Julai ya tarehe 20 2003 Klabu ya soka ya Barcelona ilimsajili na kudumu nae kwa muda mrefu katika historia yake ya soka ambako alikaa Barcelona kuanzia mwaka 2003 hadi 2008 kikiwa ni kipindi kirefu kwake kudumu katika klabu ya soka.

Ulimwengu mzima ulizidi kumtambua Gaucho baada ya kuhamia Barcelona kwa maana alizidi kudhihirisha ubora wake, naamini hata wamiliki wa PSG walijuta kumuuza.

Ndani ya klabu ya Barcelona ndio sehemu ambayo Ronaldinho alishinda karibia kila kitu, alibeba makombe mawili ya ligi ya Hispania, Baadae akatwaa tuzo ya Ballon D’or kwa mwaka 2006 lakini vile vile akabeba kombe la Klabu bingwa barani Ulaya UEFA mwaka 2006.  Heshima zaidi ziende kwa Franklin Edmundo “Frank” Rijkaard ambae alikuwa kocha wa Barcelona alimpa nafasi ya kutosha Gaucho ambako alifanya maajabu yale ambayo leo yanabaki historia katika vichwa vyetu sisi wadau wa soka na hata wasioshabikia soka. Akiwa Barcelona alifanikiwa kuitumikia michezo 145 na kufunga magoli 70 katika michezo hiyo.

Ujio wa kocha Pep Gurdiola ndani ya Barcelona haukuwa mzuri kwa Gaucho ambako alilazimika kuuzwa kwenda AC Milan ya nchini Italy aliyoitumikia kuanzia 2008 mpaka 2011 ambapo ulimwengu ulimshuhudia Gaucho akiisaidia AC MIlani ikitwaa kombe la Ligi kuu Italy Serie A msimu wa 2010/2011 na msimu huo huo Ronaldinho akaenguliwa katika kikosi cha timu ya Taifa. Ndani ya AC Milan Gaucho amecheza michezo 76 na kufanikiwa kutikisa nyavu mara 20 pekee.

Mnamo mwaka 2011 alihama AC Milani na kurudi kwao nchini Brazil kwenda kuitumikia Flamengo ambako kati ya michezo 33 alifunga magoli 15 tu. Hakuishia hapo amepita sehemu kadhaa Atletico Mileiro ambapo michezo 48 alifunga mabao 16, Ndani ya klabu ya  Quretatro alifanikiwa kufunga mabao 8 tu katika mechi 25 lakini ndani ya klabu ya  Fluminese hakufunga bao hata moja katika mechi 7 alizofanikiwa kuichezea klabu hiyo. Mpaka anatundika daluga Ronaldinho Gaucho amelihudumia soka mechi 441 na kufanikiwa kucheka na nyavu mara 167.

Timu ya taifa ya Brazil nako Ronaldinho Gaucho alifanikiwa kuitumikia michezo 97 ambako katika michezo hiyo Mbrazil huyo aliifungia timu ya taifa mabao 33 akishinda kombe la dunia pia Mwaka 2000.

Ronaldinho Gaucho ambae kwa mwaka 2006 alikuwa ni mchezaji alieingiza pesa nyingi kwa mwaka huo kwa kuingiza kiasi zaidi ya Dola milioni 19 kama endorsment tu kutokana na kufanya kazi na makampuni mengi kama Pepsi, Cocacola, EA SPorts na mengineyo.   

Kama wahenga wasemavyo KIZURI HUWA HAKIDUMU. Ilikuwa ni burudani tosha kumuangalia Ronaldinho akicheza soka katika dimba, uwezo wake wa kudrible mpira, kuuchezea kwa mbwembwe za kila aina, uwezo wa kupiga mashuti, uwezo wa kupiga pasi za mwisho kisoka tunaita Assists alikuwa balaa sana, Chenga alizokuwa anapiga pamoja na uwezo wake wa kumiliki mpira na kuweza kukimbia nao akiwapa shida wapinzani ni vitu ambavyo mimi binafsi kama Jalilu Zaid nasema kabisa kusataafu kwa Ronaldinho ni tukio kubwa katika sayari ya mpira wa miguu na hakika mimi nitakuwa na cha kuwasimulia wajukuu zangu kwamba nilipata muda wa kushuhudia kiumbe huyo wa ajabu akicheza mpira kwa kiwango bora kabisa. Nenda Ronaldinho Gaucho. Soka litakukumbuka daima.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!