Ungana na Kipande chako

January 13, 2018

Bwana Ralph Hart anasimulia: Hapo kale ilivyokuwa katika uumbwaji, wanawake na wanaume hawakuwa wametengana kama walivyo hii leo. Kiumbe alikuwa mmoja, mwenye mwili na shingo, lakini kichwani alikuwa na nyuso (sura) mbili, zenye uelekeo tofauti. Ilikuwa kana kwamba ni viumbe wawili waliogundishwa pamoja, wakiwa na jinsi (sex) mbili tofauti, pamoja na mikono minne na miguu minne.

Kwa wivu wao, miungu wa Kigiriki wakajawa wivu, kwamba kiumbe huyu mwenye sura mbili (anayeweza kuangalia mbele na nyuma), alikuwa na umakini mkubwa usiokumbwa na mshitukizo wa kitu; pia miguu na mikono minne vilimfanya aweze kusimama muda mrefu na kufanya kazi bila kuchoka. Mbaya zaidi, kwakuwa kiumbe huyu alikuwa na jinsi mbili, hivyo hakuhitaji kutafuta mtu mwingine wa kushiriki naye ‘tendo’ kwa ajili ya kuendelea kuzaana.

Siku moja kiongozi wa miungu hao alisema: “Nina mpango wa kukipunguzia nguvu kiumbe hiki.”

Ndipo akakitenganisha kiumbe hicho, na kupatikana viumbe wawili; mwanaume na mwanamke. Pamoja na hatua hiyo kupelekea ongezeko kubwa la watu duniani, lakini pia ilimfanya mwanaadamu kwa kupungukiwa kipande muhimu cha sehemu ya mwili wake, kiasi cha kumfanya awe dhaifu na mwenye kuhangaika kila uchao kukitafuta kipande chake ili kukisogeza na kukifumbata (walau) karibu, ili kujirejeshea ile nguvu yake ya asili, kurudisha utulivu na kuondoka uwezekano wa usaliti, pamoja na kuitwaa tena ile nguvu ya kusimama muda mrefu, kuwa na umakini, na kufanya kazi bila kuchoka.

Hali hiyo ya kutafutana kipande muhimu kilichoondoshwa, na kujaribu tena kujikumbata pamoja, kitu ambacho tunaona miili ya wanaadamu (mke na mume) kama vile inashindwa tena kuendana, ndio leo tunaita ‘ tendo la mapenzi’.

Kwa mtazamo wangu: ukiona kila unavyojaribu kumshika na kumfumbata karibu mwenzi wako, ili kumrejesha karibu yako kama sehemu ya kipande ulichotenganishwa nacho, lakini mwenziyo haelekei wala hashikamani – achana naye – hicho kipande pengine hakikutoka kwako. Ni kama vile, umeokota betri ya simu ya Nokia kisha ukataka kuiweka kwenye simu ya Sumsung, simu haitowaka kwa sababu umeiwekea kitu (betri) kisicho chake. Mtu wa maendeleo, akikipata kipande chake, kwa shida na raha watafikia malengo. Na mtu wa anasa kipande chake kuna sehemu kinamsubiri ili wakishaungana wanyooshane. Using’ang’anie kipande kisicho chako – kitupe haraka.

HEBU TUAMBIZANE UKWELI; mwenye kipande kisicho chake anyooshe mkono tumwone!

 

Na: Maundu Mwingizi

 


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!