Unaweza kuacha FURSA na KUSAIDIA.?

January 7, 2018

Kuna kipofu alikuwa ameketi kando mwa barabara, kwa bahati akasikia mchakato wa nyayo za mtu akipita, akasimama na kuanza kuita kama anayehitaji msaada: “Habari! Habari ndugu!”

Bwana aliyekuwa akipita, akaitikia salamu na kumsogelea karibu: “Salama ndugu, kwema?”

“Kwema ndugu,” kipofu alijibu huku akitoa pesa mfukoni na kumkabidhi mzee, “tafadhali, nina shilingi elfu mbili hapa, kuna mtu amenipa msaada, naomba unisaidie kuichenji.”

Yule bwana, kuangalia vizuri mkononi mwa kipofu, akaona si shilingi elfu mbili, ni dola 100. Akaangaza huku na kule kama kuna mtu anamwona kisha akaipokea. Akaingiza mkono mfukoni, akatoa chenji ya shilingi elfu mbili na kumpa kipofu kisha akaondoka na ile dola mia. Bwana mkubwa aliona kama nyota ya jaha imemwangukia, hakumtazama kipofu yule kwa jicho la msaada. Badala yake, akatumia mwanya huo kumdhulumu.

Ikawa hivi: yule bwana kabla hajafika mbali, akashangaa kumwona yule kipofu akimjia mbio na kumsimamisha. Kwa hofu na mashaka, akasimama. Kipofu alipomfikia, akavua miwani yake myeusi na kumwambia: “Samahani bwana, mimi siyo kipofu; ninafanya utafiti kuona ni watu wangapi wana uungwana wa kumsaidia mtu dhaifu – hata kama hawaonekani hadharani, na wangapi wana ushenzi wa kutatumia udhaifu wa mtu ili kumdhulumu – wakidhani hawaonekani. Umefeli mzee!”

Uso ukiwa umemshuka kama mbuzi, yule bwana akatoa ile noti ya dola mia na kumrudishia mwenyewe huku akisema: “Samahani kaka, ni hali ngumu tu tulizonazo.”

Kijana akachukua pesa yake na kumwonesha yule bwana upande wa pili wa barabara. Huko walikuwapo watu kama watano hivi na kamera zao, wakirekodi video ya hilo tukio zima.

Nilipoona video ya mkasa huu, nilijihisi aibu utadhani mimi ndiye yule bwana. Je, ungekuwa wewe ungefanya nini?

Maundu Mwingizi (MwanaBalagha)


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!