Unahitaji Furaha..?

January 7, 2018

UNAHITAJI FURAHA? 

HAPO zamani za kale, palikuwa na ndege. Ndege huyo, aliumbika kwa uzuri akapendeza machoni. Alipambika kwa mbawa zake zenye rangi za kumetameta, na manyoya yapendezayo. Ni kiumbe kilichoumbwa kuruka angani kwa uhuru, kikileta furaha kwa kila aliyekitazama.

Siku moja, mwanamke mmoja alimwona ndege huyu na kumpenda sana. Alimwangalia namna alivyoruka; alibaki mdomo wazi kwa mshangao, moyo wake ukisuuzika kabisa, macho yake yakiduwaa kwa msisimko. Siku moja alimwalika ndege huyo waruke pamoja angani; wakapaa angani kwa buraha. Mwanamke alizidi kumfurahia na kumhusudu ndege yule.

Lakini mara, mwanamke akawaza: kwamba, ikitokea ndege huyo akaondoka na kwenda mbali zaidi, huenda asivutiwe kuruka na ndege mwingine. Na tayari alikwishaanza kuingiwa na wivu juu ya uwezo wa ndege huyo kuruka (mbali zaidi). Akahofia kubaki mpweke.

Akawaza: ‘nitamtengenezea mtego. Akirudi kwa mara nyingine, nitamdhibiti – asiondoke.’

Yule ndege, ambaye naye tayari alikuwa amezama penzini, alirudi kwa mwanamke yule siku iliyofuata, akajikuta amenasa mtegoni; akakamatwa na kufungiwa tunduni. Ikawa kila siku mwanamke anapita akimwangalia ndege wake, na kuwaonesha marafiki zake, ambao walimsifia na kumwambia: ‘sasa umepata kitu ulichokuwa ukikihitaji sana.’

Pamoja na hayo, mabadiliko yakaanza: kwakuwa tayari amekwishamdhibiti ndege wake, hakuona tena haja ya kumsisimua na kum’hengahenga, akaanza kupoteza mvuto naye. Ndege naye, kwa kushindwa kwake kuruka na kupoteza maana halisi ya maisha yake, akaanza kuchoka, hata manyoya yakapoteza umetevu na mvuto; akabadilika na kuwa mbaya. Kufikia hapo, na mwanamke naye, ukiondoa kumsafishia na kumwekea chakula tunduni, hakujishughulisha naye zaidi.

Siku moja, kwa kihoro na adha za kupoteza uhuru wake, yule ndege akafa. Mwanamke alihuzunika mno. Kila mara alimwazia ndege wake kwa simanzi. Hakumuwaza alivyokuwa amedhoofu tunduni, bali alimuwazia siku walipokutana kwa mara ya kwanza na kuruka angani pamoja.

Lau angejitafakari kiundani, angetambua kwamba, kilichompendeza na kumsisimua kwa ndege yule, haikuwa mwonekano wa mwili wake awapo tunduni, bali kule kupendeza kwake kuliko sababishwa na ile furaha iliyotokana na ule uhuru aliokuwa nao; nguvu za mbawa zake arukapo angani.

Kwa kihoro cha kumkosa ndege, maisha ya mwanamke yakapoteza maana. Punde, naye kifo kikamgongea hodi.

Kisa hiki nilichosimuliwa na babu yangu, mzee Paulo Coelho, katika kitabu chake cha Eleven Minutes, kimenifikirisha sana juu ya umuhimu wa kujifunza kuheshimu uhuru halali wa uliye naye. Usiogope kumpoteza kwa kumwachia uhuru wake. Na hata asiporudi; kwanza haukumuumba wewe – si mali yako. Chambilecho mzee Paulo Coelho, hakuna awezaye kupoteza mtu, kwa sababu hakuna anayemmiliki yeyote. Na hiyo ndiyo siri kuu kuhusu Uhuru na furaha: yaani, kuwa na kitu muhimu duniani bila ya kukimiliki.

Ukipenda boga, penda na ua lake. Umemkuta mtu anaishi kwa kufurahiana na rafiki zake, ghafla shangingi umemdhibiti – hutaki acheke nao wala ataniane nao tena; umemkuta mtu anatembeleana na nduguze, ghafla jini mkakamba umemdhibiti hutaki atoke kwako. Kumnyima uhuru wake ni kumharibia haiba yake iliyokufanya ukavutiwa naye. Ukimpoteza, nawe utaangamia.

Maundu Mwingizi (MwanaBalagha)


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!