Siku nimekutana na msichana mrembo kwenye Mwendokasi.

January 7, 2018

Wakati naperuzi katika mitandao ya kijamii kule Twitter ambao ni mtandao ninaokubali sana kwa sababu si tu unaniongezea maarifa zaidi bali pia umenipa marafiki wengi ambao baadhi yao sasa hivi tunaishi kama ndugu tofauti na mitandao mingine nimekutana na tweet ya jamaa yangu mmoja ambapo aliandika “Madada wanaofanya kazi POSTA wanaringa kinyama…unaeza sema wote wanafanya kazi IKULU!!! Baada ya kuisoma ikanikumbusha kisa kimoja ambacho kiliwahi kunitokea mie katika jiji hili la lawama. Kama hujabahatika kufika Dar Es Salaam Posta ni eneo ambalo kuna Ofisi nyingi na zenye hadhi ya juu baadhi lakini zingine ni za kawaida pengine kuliko hata hiyo Ofisi unayofanya kazi wewe katika mkoa mwingine. Kama wewe unapafahamu basi utakuwa shahidi wangu katika kile nilichosema. Mara yangu ya kwanza kufika wacha wee.!! Na ushamba wangu ilibidi niyape macho yangu faida tu nishangae majengo na mpangilio mzuri wa mazingira pamoja na usafi wake. Kwa kweli panavutia sana.
Basi bhana sikumbuki ilikuwa ni siku gani nilipokutana na kisanga cha mdada anaefanya kazi huko Posta kwenye ofisi moja nzuri kweli kweli (Jina kapuni). Kuanzia mida ya saa Kumi alasiri Kituo cha Mwendokasi cha Posta ya Zamani kashi kashi huwa ndo zinaanza kwa sababu watu wengi huwa ndo wanatoka kazini na kama nilivyosema mwanzo Posta kuna Ofisi nyingi hivyo watu wanakuwa ni wengi ingawa sio sana kwa sababu ndo mida watu huanza kutoka Maofisini wanakuwa wengi zaidi kituoni kuanzia saa 10 kwenda mbele. Mie nilibahatika kukata tiketi yangu saa 9 na vidakika kadhaa hivyo Mabasi ya kwenda Kimara Terminal nilikuwa naweza kubahatika hata kupata nafasi ya kukaa. Basi bhana wakati nakata tiketi akatokea mdada mmoja mzuri kweli kweli ambae kila Kijana mwenye kuhitaji mrembo basi hakika asingesita kumsumbua yule dada. Akili yangu hata haikuwaza sana kuhusu uzuri wake bali mimi nikawa bize na simu yangu nikiperuzi mitandaoni kujua kilichojiri kutokana na ubize niliokuwa nao kutokea asubuhi huko mjini kwenye mizunguko yangu mwenyewe.
Mdada nae akakata tiketi yake vyema kabisa akajongea kuja sehemu ya kupanda gari akasimama karibu na mimi. Alikuwa amevalia nguo maridadi kabisa zenye kumpendeza mwenzenu nilikuwa nimevaa zangu Pensi, Sandals na Tisheti yangu pamoja na Begi lililokuwa na vitu vyangu. Gari likaja kutoka kituo kikuu cha Mabasi ya Mwendokasi Kivukoni likiwa na nafasi chache za kukaa kiasi zisingeweza kututosha wote tuliokuwa tumesimama pale kulisubiria kwa hivyo kilichokuwa kimesalia ni kila mtu kutumia nguvu zake kupata sehemu ya kukaa. Mara nyingi huwa sipendi kutumia nguvu kusukumana hasa sehemu wanapokuwa Kina Mama na Watu wazima ambao naona kabisa wana hadhi ya kuwa wazazi wangu hivyo huwa najituliza tu. Basi nikawafanikiwa kuingia kwenye gari ila sikubahatika kupata nafasi ya kukaa ikabidi nisimame, bhana nikajikuta sehemu nimesimama kumbe pale pale ndo yule msichana amepata sehemu ya kuketi ameketi tu akiwa ameshikilia simu yake nzuri aina ya Iphone wenyewe vijana wa sasa wanaziita Tunda. Nikamsabahi “Mambo” hakujibu kwa kuongea bali akatumia ishara ya mkono na kunionesha dole gumba kwa maana ya kwamba “Safi au Poa” nikaridhika kabisa bila shida. Alikuwa ameketi na Mama mmoja pembeni nikaona isiwe taabu kwa mama ikabidi nimuombe kijana mwenzangu anisaidie Begi langu (Kama ambavyo huwa tunafanya mara nyingi mtu ambae amepata sehemu ya kukaa ukiwa umechoka unamkabidhi mtu Mzigo wako akusaidie wewe umesimama) na mie ikabidi nimwambie dada “Samahani dada naomba unisaidie begi langu” Mdada hakujibu chochote akaacha kufanya alichokuwa anafanya kwenye simu yake na kuinuka kuniangalia vizuri akaniangalia kuanzia kichwani mpaka miguuni. Cha kumshukuru Mungu miguu haikuwa na vumbi kwa sababu kule Posta bwana vumbi hamna sehemu kubwa. Baada ya kuniangalia akashusha macho yake kuyaelekeza kwenye uso wa simu yake bila kuongea kitu chochote zaidi ya “KUSONYA” kwa kweli niliumia moyoni mpaka nikajisemea si heri tu angesema amechoka au hataki nijue.? Kuliko kunisonya mtu mzima mie. Nikaona sawa kwa sababu maisha ni kuchagua tu pengine kaniona nilivyo akaona siko kwenye viwango vyake ndo kaamua kufanya hivyo au labda na yeye amechoka ila hajataka kusema. Lakini kwanini asonye.? Ni ishara ya DHARAU au ni nini.? Sikupata jibu.
Basi likakata barabara weee mpaka Kimara Terminal sehemu ambayo kila mtu anapaswa kushuka na kukata tiketi kwa ajili ya kuelekea Mbezi Louis (Kwa wale ambao hawana Kadi za Mwendokasi) Wenye kadi huwa ni kufikia tu kwenye Foleni na kusubiri kuingia kwenye gari. Ikabidi tukimbizane sie tusokuwa na kadi tujipatie tiketi tuwahi foleni. Kumbe yule mdada nae alikuwa kama mimi inabidi akate tiketi na yeye ili aweze kupanda gari. Karibu na sehemu ya kukatia foleni akasimama akipekua mkoba wake kutafuta pochi ili alipe apate tiketi na yeye nikashindwa kujua kwanini kama amepigwa na bumbuwazi ikabidi nisiende mbali nae nijue kunani, Kama mjuavyo pale mtu ukisimama sehemu zaidi ya sekunde 30 unaonekana usumbufu zikasikika sauti za wanaume kwa vijana na wamama “Wewe shida nini pisha hapo au rudi nyuma” Nikaisikia sauti ya unyonge kutoka kwake akisema “Nimesahau Pochi Ofisini” Sikutaka kusubiri ikabidi nikimbie kwenye foleni ya tiketi nikakata tiketi Mbili moja yangu na nyingine ya kwake. Nikarudi alipokuwa amesogea pembeni bila hata kumsemesha nikamkabidhi tiketi moja akaipokea na mimi bila hata kusubiri ahsante nikawahi foleni ya Gari nikafanikiwa kupanda gari nikaenda mpaka mwisho kule sehemu ambayo nilijiaminisha hawezi kuja kukaa huko kwa sababu alionekana ni aina ya wale wasichana wasiopenda kujipa taabu. Nikamuona na yeye anaingia kwenye gari lile lile nililopanda mimi ila nikaona kabisa macho yake akiyaangaza kuona nimekaa sehemu gani nikafanya kusudi kujikinga usoni na Begi langu asinione na uzuri kule nyuma nafasi zilikuwa zimeshajaa hivyo asingeweza kuja kukaa huko.
Safari ya kuelekea Mbezi ikaanza kwenye Gari nikiwa nasoma kitabu kinaitwa Who Will Cry When You Die kilichoandikwa na mwandishi mmoja matata sana Robin Sharma moja ya vitabu bora kabisa nilivyowahi kusoma. Hiki ni kitabu kinachofundisha ni kwa jinsi gani uishi na wanadamu hapa duniani ili siku ukiondoka basi wapate kukusema kwa mema yako na kuyaenzi.
Safari iliendelea mpaka Mbezi Louis ambako ndo ilikuwa mwisho wa safari yetu nikiamini hata yule dada alikuwa anaishi kule. Alitangulia yeye kushuka kwenye gari na mie nikafuatia. Sikuamini macho yangu nikakuta amenisubiri hapo chini nikajifanya kama sijamuona nikataka kuvunga ili niende nyumbani bila kumsemesha maana mimi huwa nina kasumba moja maishani mwangu “Ukinionesha dharau mie huwa nakupuuza” Yule dada kabla sijaondoka akavuta mkono wa Begi langu na mimi nikageuka kwa mshangao maksudi mazima. Nikamuuliza “Vipi mbona kuvutana.?” Akasema “Samahani sana kwa kilichotokea kwenye gari mwanzo na pia nashukuru kwa kunipatia tiketi ubarikiwe” Nikamjibu. “Haina shida lakini katika maisha haya usijione bora dada” Baada ya kufahamiana majina na kubadilishana mawasiliano akaniambia “Nilitakiwa kushuka KIbanda cha Mkaa ila nikalazimika kuja mpaka hapa Mbezi ili niseme niliyoyasema Ahsante” Na mimi sikutaka kumpa muda mrefu wa kusimama nae pale basi nikahakikisha nampa kinachoweza kumfikisha Kibanda cha Mkaa na mie nikaondoka kuendelea na harakati zangu. Pale Mbezi huwa kuna ngazi jioni jioni watu huuza vitu mbali mbali mpaka nafika hapo mdada wa watu alikuwa bado amesimama akiangalia hivi huyu ni mtu wa aina gani au ni jini kumbe hapana ni mtu tu wa kawaida. Sikutaka kufuatilia zaidi kama amesimama nusu saa au mwaka mzima pale nikaondoka zangu nikaja kupokea meseji usiku kwamba “Nilifanikiwa kufika home salama Jalilu Mungu akubariki sana” Sikujibu kwa siku hiyo. Mpaka sasa naandika hii stori yule dada tunaheshimiana sana nimekuwa kama kaka yake akiwa na jambo analohitaji ushauri basi sisiti kumshauri na nikiwa na jambo ambalo linafaa kumshirikisha basi siachi kufanya hivyo.
TANBIHI: Katika maisha haya tunayoishi kila siku usijione wewe ni bora kwa sababu ya sehemu uliyojiajiri au ulipoajiriwa au kutokana na mavazi uliyoyavaa basi kuona watu wamevaa tofauti na wewe unawadharau na kuwaona hawana thamani kwako wakikuuliza jambo basi wajibu kwa staha na heshima maana kwa Mungu hakuna mbora ila mwenye kumcha yeye na kuishi na watu kwa wema.
KUMBUKA: “When you were born, you cried while the world rejoiced. Live your life in such a way that when you die, the world cries while you rejoice.”

Na: Jalilu Zaid


Comments

  1. Jane - January 8, 2018 at 7:32 am - Reply

    What a story… Hongera kwa kuwa positive na kuspread positive vibes. This spoke to my heart ““When you were born, you cried while the world rejoiced. Live your life in such a way that when you die, the world cries while you rejoice.” Thank you for sharing.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!