Mwanamke sio sehemu ya kufanyia mazoezi ya ngumi.

January 7, 2018

Jua kali la Dar Es Salaam lililoambatana na joto ndio hali halisi iliyopo kwa sasa katika Jiji hili lililojaa lawama za kila namna kila mtu yuko bize na harakati zake hana muda na mwenzake kila mtu anakimbizana kutafuta ridhiki yake mwenyewe.
Siku ya Ijumaa ya leo imeniachia mengi kichwani mbali na mizinguko ya hapa na pale lakini kuna kero moja nimeipata ambayo si mbaya nikawashirikisha wasomaji wangu ambao nimewasahau kwa muda.
Mida ya saa Tisa Unusu kuelekea saa 10 kwa Dar Es Salaam huwa ni muda wa fungulia fujo kwenye daladala ambapo watu huwa ndo wanaanza kutoka kazini hivyo usumbufu kwenye magari huwa ndo unaanza anza hasa ukiwa unapandia kwenye vituo vya kati kati. Kwa hali nilivyoiona nikaona si mbaya kupanda Gari kutoka Mwenge mpaka Mawasiliano Sinza ili nipate usafiri wa moja kwa moja usio na usumbufu. Mungu si Athumani nikabahatika kupata usafiri. Sehemu nilipokaa mimi akaja kukaa mama mmoja ambae alikuwa na mtoto mdogo kwa kukadiria umri wake ni miaka minne hivi na masiku kadhaa. Mama huyo alivyokuwa amevalia vyema kitenge chake maridadi kabisa mtoto nae alikuwa mchangamfu kweli kweli. Binafsi huwa napenda sana kutania tania watoto kwa ajili ya kuwaona wakiwa na furaha. Yule mtoto alionekana mtundu na mkorofi kwa dakika hizo chache nilizokaa nao kwenye gari mpaka akaninyima fursa ya kumtania tania ikabidi nikaushe tu kimya. Yule mama alikuwa amefungwa Bandages kwenye jicho kikiwa ni kiashiria kuna kitu kilimtokea na ilionekana dhahiri hakuwa na muda mrefu ametokewa na kitu hicho kibaya ambacho kwa mwanzo sikukijua ni nini. Kama ilivyo kanuni ya maisha yangu huwa si mwepesi wa kuuliza matatizo ya mtu kwa sababu huwa ninaamini kumuuliza matatizo yake mtu kunaweza kusababisha uchungu na maumivu akikumbuka mambo hayo.
Nilikuwa nimeweka Airphone zangu nikisikiliza ushairi mzuri wa Kiswahili nikalazimika kuzitoa ili nifanye udadisi wangu pamoja na busara kubwa niweze kufahamu ni nini kisa na mkasa kilichomkuta yule mama.
Duniani kuna watu wenye mioyo ya tofauti wengine Bahili na wengine wamejaaliwa roho ya kutoa katika kile alichoruzukiwa. Basi ndo kitu nilichoshuhudia leo na kupitia Utoaji ndo kumenipa mwangaza wa kufahamu kisa kilichomkuta yule mama. Baba mmoja ambae alipanda daladala kituo kama cha Saba hivi kutoka stendi kuu ya Daladala Sinza alilazimika kusimama kutokana na Gari kujaa. Wakati tunakaribia mwisho wa safari yetu yule Baba akatoa kiasi fulani cha hela na kumpatia yule mtoto mdogo ambae alikuwa amebebwa na mama yake aliekuwa na Bandage usoni. Mama mtoto alionekana kufurahi sana hasa pale wakati anamwambia mwanae aseme ahsante kwa kile kiasi alichopewa “Chukua mwambie mama akununulie maziwa” ndio maneno yaliyomtoka yule baba wakati akimkabidhi mtoto yule kile kiasi cha hela.
Mama wa mtoto alionekana kufurahi sana kiasi uso wake ukaonesha dhahiri yuko tayari kushirikisha mtu kilichomsibu. Yule baba nae kumbe alikuwa na wazo kama langu la kuhitaji kufahamu kisa kilichomtokea mama yule. Akamuuliza kwa kauli ya kiutu uzima “Pole sana Dada Tatizo ni nini limekupata”.? Hapo ndo nikayasimamisha masikio yangu kwa weledi mkubwa ili nijue kitu gani kilichomsibu nikamsikia mama akijibu “Mume wangu kanipiga kidogo lakini sio shida kubwa”. Ndio kuna rafiki yangu aliwahi kunambia akina mama ni wavumilivu sana. Kupitia huyu mama pia nimeona ni kwa namna gani wanavumilia. Fikiria kipigo alichopewa lakini bado anasema ni kawaida tu hakuna shida.
Bwana kuna tabia mbovu ambazo ziko katika baadhi ya watu ambapo mwanaume kumpiga mke wake ni mambo ya kawaida. Mimi labda niulize swali. “HIVI HUWA KUNA MANUFAA GANI KUMPIGA MPAKA KUMUUMIZA MWANAMKE”.?
Imenisikitisha sana.
Natoa wito kwa wanaume wenzangu ambao wana tabia hizi za ukorofi kumpiga mwanamke mpaka damu sio tabia nzuri hata vitabu vya dini haviruhusu kukitokea utofauti wowote katika mahusiano yenu ya ndoa malizeni matatizo hayo chumbani msiruhusu watoto wakajua kuwa kati ya baba na mama kuna utofauti maana hiyo mnawatengenezea chuki baina yenu.
TANBIHI: Wanawake wasitumike kama sehemu ya kufanyia mazoezi ya ngumi.

Na: Jalilu Zaid.

 


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!