Dhana ya Ukahaba katika kitabu cha “ELEVEN MINUTES”

January 7, 2018

Katika kitabu hiki, kilichopewa namba 97-8-0-00-716605-3, mwandishi Paulo Coelho, anatumia kalamu kuzungumza na ‘watu wazima’ kuhusu malezi na athari zake, mapenzi na faraja yake, ngono na mizungu yake, ukahaba na matokeo yake. Kwa minajili hiyo, haitakuwa murua kitabu hiki kusomwa na watoto wadogo. Hii ni kwa sababu, humo ndani mwandishi amefunguka┬ákinagaubaga juu ya ladha na adha zitokanazo na tendo kuu la ngono. Namna msisimko wa ladha usababishwao na upevukaji wa binti, unavyoweza kuathiri maisha yake endapo hatopata mtu wa kumweka chini na kumnasihi. Hata uchambuzi huu pamoja na kujaribu kutumia sana tafsida, bado mchambuzi anawanasihi watoto pamoja na ‘watakatifu’ wote kutokuusoma.

Tuanzie hapa: Akiwa ameharibikiwa mambo ugenini, Geneva, Uswisi, Maria (binti toka Brazil) aliamua kuomba kazi ya ukahaba katika club maarufu ya Copacabana. Na baada ya mmiliki kuridhishwa naye, alikabidhiwa kwa mmoja kati ya makahaba toka Brazil pia, ili apewe ushauri. Baada ya maswali ya hapa na pale, ushauri wa kwanza aliambiwa:
“Sikia, nirahisi tu, unapaswa kuzingatia kanuni tatu za msingi: “Kwanza: usiangukie mapenzini na yeyote unayefanya naye kazi wala utakayefanya naye ngono. Pili: kamwe usiamini ahadi yoyote utakayopewa na hakikisha malipo yanafanyika kabla ya tendo. Tatu: usitumie kilevi.”

Baada ya ukimya, kahaba akaendelea kutoa somo: “Na, hakikisha hii kazi unaianza leo. Endapo utarudi nyumbani usiku huu bila ya kuhudumia walau mteja mmoja, wazo la pili la kughairi litakujia, na hautokuwa na ujasiri wa kurudi tena.”

Kimsingi, japo ni kweli Maria alidhamiria kufanya kazi hiyo, ila usiku huo alifika hapo Copacabana kwa ajili tu ya kufanya utafiti kabla ya kuamua kuingia rasmi. Lakini kwa maelezo ya ushawishi aliyoambiwa, akajikuta amekubali kuanza kazi usiku huohuo. Mwandishi anatuonesha namna ilivyo hatari kukurubia jambo ovu; nguvu ya ushawishi wa uovu ni kama kuchanganya maji safi na matope, yote takuwa matope tu.

Baada ya Maria kukubali, Coelho anaendelea kutusimulia kwamba, yule kahaba alimfuata Milan (mmiliki wa club) na kurudi naye mezani kumalizia kumpa sheria Maria. Swali la kwanza la Milan kwa Maria likawa : “Je, umevaa kocho nzuri?”

Baada ya Maria kujibu, Milan alimwelezea aina ya kocho atakayopaswa kuvaa kuanzia siku inayofuata. (Kama ulikuwa hujui, kocho maana yake chupi). Kisha akaendelea kumpa sheria nyinginezo. Namna ambavyo biashara inaendeshwa hapo, ni rahisi tu. Mteja akiingia ukimbini, akivutiwa nawe atakufuata mezani na kukuuliza, “Je, utahitaji kinywaji?”
Ambapo Maria atapaswa kujibu NDIYO au HAPANA. Alipewa uhuru wa kuchagua mtu wa kuondoka naye, japo hairuhusiwi kukataa zaidi ya mara mbili kwa usiku mmoja. Na endapi atamkubali mteja atakayemfikia, atapaswa kuagiza ‘fruit juice cocktail’ ambacho ndicho kinywaji ghali kuliko vyote hapo Copacabana. Marufuku kuagiza kilevi wala kuruhusu mteja akuchagulie kinywaji atakacho yeye.

Baada ya kinywaji, anaruhusiwa kuingia kati kucheza mziki na mteja wake, na baada ya kurudi mezani, ndipo Maria anaweza kukubali kuondoka na mteja wake kwenda hotelini alikofikia kumpa huduma (ngono). Bei ni Francs 350 ambapo Francs 50 anachukua Milan kama malipo ya meza yake (neno ‘malipo ya meza’ ni mbinu tu ya kukwepa kutuhumiwa na/au kukamatwa kwa kuwatumikisha wasichana kingono). Pia, ni marufuku kwenda nyumbani kwa mteja wala kwenda naye kwenye hoteli yenye hadhi chini ya nyota tano. Kama mteja hana pa kukupeleka, kuna hoteli maalumu jengo kama la tano toka hapo Copacabana, na ni lazima kutoka na taxi ili wasionekane.

Kabla hawajaachana kwa ajili ya Maria kuanza kazi rasmi, Milan aliongezea: “Nilisahau kitu, muda unaopaswa kutumika tangu kuagiza kinywaji mpaka kuondoka na mteja, haupaswi kwa namna yoyote ile, kuzidi dakika 45. Kumbuka ninalisha na kusomesha watoto kwa kutegemea kazi hii.”

Hapakuwa na sababu ya kumwogopa mteja yeyote. Polisi na idara ya afya, kila mwezi, walichohitaji ni kuchukuwa sample ya damu ili kujihakikishia kwamba, makahaba hawana magonjwa ya ngono. Hivyo ndivyo biashara haramu zinavyolindwa na mifumo ya kifedhuli kiasi cha kuchipua na kushamiri kana kwamba ni biashara halali. Zaidi, matumizi ya kinga kwa kila tendo ilikuwa ni lazima, ingawaje hapakuwa na njia ya kuhakiki kama sharti hilo linafuatwa. Hapo si nimeeleweka? Ndo hivyo.

Mwandishi anasema: Maria, kama ilivyo kwa makahaba wengine wote, naye alizaliwa bikra na asiye na hatia. Kipi basi kilimfanya hata akajikuta akitoka kwao Brazili hadi Uswisi na kuangukia katika nakama hii? Mwandishi amekiandika kisa hiki, kwa mtindo wa moja kwa moja, yaani, tangu kukua kwa Maria na kubadilika kwake kitabia. Ila mimi nimeamua kukianzia katikati kisha endapo kama nitapata wasaa, basi nitarudi nyuma kukuelezeeni mapito yake ya utotoni.

“Je, utahitaji kinywaji?” Naam, hatimaye Maria alipata mteja wa kwanza, akakubali; mara mteja wa pili, akaenda naye; mara watatu; hatimaye akazoea kazi. Kupitia kwa makahaba wenziye alijifunza jambo moja ‘adhimu’, kwamba, ‘Ukahaba si sawa na biashara nyinginezo. Huku ukiwa ndio unaanza (mahaba mpya), upata wateja (pesa) wengi zaidi na kadiri unavyokuwa mzoefu ndivyo unavyoambulia kidogo. Hivyo, ni lazima kila siku kujifanya u-mgeni wa fani mbele ya mteja (mwanaume). Na moja kati ya ushauri wa muhimu, japo wa ajabu kidogo, Maria alipewa na Nyah (kahaba mwenziye) aliambiwa: “Mteja wako akikaribia kufika ‘kileleni mwa mlima’, lazima uhakikishe unanung’unika sana kana kwamba mmefika kileleni pamoja.”

Wakubwa mmenielewa? Inashangaza eenh? Hata Maria alistaajabu vivyo hivyo, akamuuliza Nyah: “Kwanini nifanye hivyo ilhali mteja ndiye analipia raha yake mwenyewe?”

Nyah akamjibu: “Hapana, utakosea ukiamini hivyo. Iko hivi, Mwanaume hajithibitishi urijali wake kwa ‘jogoo kupanda mtungi’ tu. Bali hujihisi yu-mwanamume kamili kwa kuhakikisha anamridhisha mwanamke. Na kama atajiona ameweza kumridha mpaka kahaba, hapo hujiona yeye ndiye kidume wa dunia nzima.”

Umeona sasa udhaifu wa wanaume? Kwahiyo basi, kwa kuzingatia somo hilo la ulaghai, kahaba huiteka akili ya mteja wake na kujipatia malipo zaidi ya ile Francs 350. Maria alilizingatia hilo na kufanikiwa kuwateka akili wanaume wengi. Bila shaka hapa, mwandishi anawafunda wanawake namna ya kuitambua saikolojia ya wanamume na namna walivyo mabahau wa hisia zao wenyewe. Mbali ya hilo, uzoefu mwingine alioupata Maria katika kazi yake, alikuja kugundua jambo lilomshangaza sana, kwamba mmoja kati ya kila wateja wake watano aliokwenda kuwahudumia, hutokea kutohitaji ngono wawapo chumbani. Mtu anakuja club, anakutaka, analipia gharama zote na baada ya kucheza muziki anaondoka nawe mpaka hotelini kwake, lakini unapofika muda wa wote kubaki watupu, mteja (mwanaume) husema hakuna ulazima wa ngono, na kwamba wangeweza tu kupiga soga na kujadili maisha; faida na hasara za kazi, au kuhusu upweke wao katika familia zao, au kuhusu wake zao kukosa uaminifu ndani ya ndoa, au kuhusu kukosa furaha na kukosa watu wakuzungumza nao, nk. Kumbe wako wanaume wengi wananunua makahaba si kwa hitaji la ngono, bali misongo na matatizo mengi ya kisaikolojia huwafikisha hapo. Bila shaka Paulo Coelho ameamua kuifunulia jamii pazia kubwa juu ya kile ambacho haikijui.

Mbali na ukahaba, Maria alikuwa ni msomaji mkubwa wa vitabu. Na tangu alipozuru kwa mara ya kwanza hapo Geneva, akitokea kwao Brazili, alishikana urafiki na mkutubi wa moja kati ya maktaba za hapo Geneva. Mara nyingi alifika hapo maktaba, akasoma na kuazima vitabu. Hivyo, baada ya kuona haja ya kuwa na ufahamu mpana wa matatizo yanayofanana kwa baadhi ya wateja wake, alirudi tena maktaba na kuanza kuazima vitabu mbali mbali; siasa, mahusiano, saikolijia, biashara, nk. Hiyo ikawa inamrahishia kutoa ushauri kwa wateja wake waliokuwa wakikwepa ngono na kuhitaji kupinga soga. Kulifanikisha hilo, kukamfanya apendwe na wateja wengi na kuongezewa takrima mbali ya malipo ya yale msingi (350 francs).
Mwandishi amefanya utafiti wa kutosha katika kitabu hiki. Bila shaka, kwa namna alivyofunguka kitaalamu, lazima aliwatafiti vya kutosha makahaba kabla ya kukiandika.

Mbali ya kupenda kujisomea vitabu, Maria pia alikuwa na utamaduni wa kuandika kila nukta ya mapito yake maishani katika shajara yake (diary). Na moja ya maandiko yake, yalisomeka hivi: Wanaume wote; awe mfupi au mrefu, kiburi au muungwana, mcheshi au mpole, wanafanana tabia moja; wakija club (kuwinda wanawake) wote huwa ni waoga. Wale wazoefu, huficha hisia zao kwa kupaza sauti huku na kule, na wengine kunywa pombe ili kufukuza hofu, lakini wote ni waoga. Hivi wanaume wanaogopa nini? Maana mimi ndiye niliyepaswa kuogopa kwani ndiye ninayetoka eneo langu la kazi (club) na kumfuata yeye hotelini kwake.

Unajua anachomaanisha Maria? Iko hivi:

Mwandishi anasema, mwanaume anapokwenda dukani, mathalani kununua viatu. Ikitokezea kiatu hakijamridhisha, basi atarudi kwa muuzaji, kifua mbele kuvirudisha na hata kudai sehemu ya fidia. Cha ajabu, mwanaume huyo huyo ‘akimnunua kahaba’ na ikatokea wakiwa faraghani jogoo akashindwa kupanda mtungi, mwanaume atapagawa kwa kukosa raha na amani, na hata kutokurudi tena katika club aliyomtoa mwanamke huyo ili kukwepa aibu ya kukutanisha naye macho. Woga mtupu. Maria anasema: “Ni mimi ndiye niliyepaswa kuhisi fedheha kwa kushindwa kutimiza jukumu langu la kumsisimua mteja wangu mpaka ashituke, lakini ajabu mwanaume anajilaumu mwenyewe.”

Badala mwanamke ajiulize ana kasoro gani hata mteja wake ameshindwa kusisimka, cha ajabu (mteja) anahangaika kujichunguza kama analo tatizo binafsi.

Kwa jicho la kahaba huyu, wanaume wameonekana ni viumbe wa ajabu mno. Yaani pamoja na ushujaa wao, mijiguvu ya kufanya kazi, uwezo wa kushughulikia misongo ya mawazo, wazuri kwa ushauri, nk, wanajikuta wakiishia kwenye club kununua makahaba wa kulala nao kwa tendo la usiku mmoja tu. Tena si tendo la usiku mmoja basi, ni takribani ndani ya dakika kumi na moja tu, naam ‘eleven minutes’. Ukitoa muda wa kupiga soga, kucheka, kuhamasishana, kusukuma gari kama stata ina matatizo, kuvua na kuvaa nguo, utakuta muda unaotumika kwa tendo lile tu la kupanda na kushuka mlima, ni takribani dakika kumi na moja tu. Ndo maana kitabu hiki kikaitwa ELEVEN MINUTES kuashiria dakika chache zitumikazo tendoni. Ukisikia mkeo anakwambia naomba ‘eleven minutes’ yangu ndo umwelewe sasa.

Mwishoni mwa kitabu hiki, kuna raha na msisimko wa ajabu. Kwa kukuibieni siri tu ni kwamba, Maria ataachana na ‘wateja’ na hatimaye kupata mpenzi ambaye alikuwa anaijua vema kazi afanyayo Maria. Je, itakuwaje? Kanunue kitabu ujisomee mwenyewe.

Maundu Mwingizi (MwanaBalagha),


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!